Serikali yapongeza JUWANATA kwa kuanzisha Jumuiya ya wasindikaji nafaka.

Serikali imeupongeza uongozi wa muda wa Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka Tanzania (JUWANATA) kwa kukamilisha rasimu ya katiba ya umoja wao. Pongezi hizo za serikali zimetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Masoko toka Wizara ya Kilimo Benito Kavenuke wakati wa mkutano maalum wa Juwanata uliofanyika Jijini Dar es Salaam.


“Serikali inaunga mkono Juwanata kwa kutekeleza kwa haraka azimio la mkutano wa Waziri wa Kilimo na wafanyabiashara wa nafaka la kuanzisha jumuiya ili kutatua kero ya ukosefu wa masoko ya bidhaa zitokanazo na mazao ya nafaka.” alisema Kavenuke.


Awali akitoa taarifa ya mkutano huo maalum,Mwenyekiti wa muda wa Juwanata Oscar Munisi alisema lengo la jumuiya ni kuitikia kwa vitendo kauli mbiu ya serikali ya kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao ya nafaka . Munisi aliongeza kusema jumuiya yao inaundwa na wanachama wamiliki wa viwanda vya kusindika nafaka na mafuta toka mikoa yote ya Tanzania bara ambapo kazi ya kuandaa katiba ya muda ilishirikisha wadau wote.


Kwa upande wake Meneja Mradi wa Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki (EAGC) Ikunda Terry amewataka wasindikaji hususan wa mchele kuongeza ubora ili kufikia soko kubwa la nchi za Uarabuni. “Tanzania ina fursa ya soko la uhakika la mchele kwani sasa uzalishaji umefikia tani 2,200,000 wakati matumizi ya ndani kwa mwaka ni kama tani milioni moja,kwa hiyo tunayo ziada ya tani milioni moja kwa ajili ya kuuza nje ya nchi” alisisitiza Ikunda.


Kufanyika kwa mkutano huu maalum kunafuatia mkutano wa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alioitisha hapo tarehe 29 na 30 Agosti mwaka huu kujadili changamoto za masoko ya mazao ya nafaka nchini.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa