Bajeti ya Kilimo Tanzania-umwagiliaji na mbegu bora zapewa kipaumbele

Idadi ya Watanzania ni Milioni 61.74.  Kati ya hao asilimia 65.6 sawa na  zaidi ya Watanzania milioni 40 maisha yao ya kila siku yanategemea sekta ya kilimo moja kwa moja na Watanzania wote Milioni 61.74 wanahitaji chakula.

Umwagiliaji na mbegu bora ni mojawapo ya sekta zilizopewa kipaumbele katika Bajeti ya Kilimo ya mwaka huu nchini Tanzania. Wizara ya Kilimo imefungua ofisi 121 za wilaya za umwagiliaji na kuajiri wataalam 320 ambao hivi sasa wamepangwa katika wilaya kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao. Vilevile, tarehe 20 Machi 2023, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua na kugawa magari 53 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za umwagiliaji ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli.

“Kihatarishi namba moja kwa taifa letu itakuwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula na hivyo kuhatarisha uimara

wa uchumi wetu na usalama wa Taifa letu. Ili kuwa salama kwenye eneo hili ni lazima kuendelea kuwekeza katika mifumo imara na himilivu ya kilimo inayotumia teknolojia za umwagiliaji za kisasa, uwezo wa kuhifadhi mbegu zetu za asili ili kuwa msingi imara wa kufanya utafiti kupata teknolojia bora za uzalishaji wa mbegu ili kujihakikishia usalama wa chakula na ulinzi wa uchumi wetu,” alisema Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Bajeti hiyo ilimulika mambo kadhaa ikiwemo;

  1. Kuimarisha utafiti
  2. Kutoa ruzuku ya mbegu za alizeti, ngano na miche ya chikichi
  3. Kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo
  4. Kuimarisha na kutoa huduma ya upimaji wa afya ya udongo
  5. Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji
  6. Kuimarisha huduma za ugani na kuhamasisha kilimo cha ukanda kutokana na ikolojia za kilimo
  7. Kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo
  8. Kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa Mitaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo
  9. Kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya kilimo
  10. Kuhamasisha na kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja
  11. Kuanza kutoa ruzuku ya mbolea mwaka 2022/2023
  12. Kuimarisha Kilimo Anga; na
  13. Kuimarisha maendeleo ya ushirika.

 Baadhi ya mipango ya serikali kama ilivyoasirishwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe mbele ya Bunge ni;

  • Serikali itaajenga nyumba za maafisa Ugani wa kilimo katika kata 4,000 nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakulima.
  • Wizara kupitia Tume itachimba visima kwa ajili ya wakulima 150 kwa kila Halmashauri ambao ni sawa na jumla ya wakulima 27,600 katika Halmashauri 184. Wakulima hao watapatiwa vifaa vya umwagiliaji (irrigation kits) kwa ajili ya kuhudumia ekari 2.5, tenki la maji la lita 5,000 na kuwawekea mfumo wa sola ambapo jumla ya ekari 69,000 zitaendelezwa kwa uzalishaji wa mazao ya nafaka, mbogamboga na matunda.
  • Katika mwaka 2023/2024, Wizara kupitia TARI imepanga kufanya utafiti wa mbegu aina 10 za  mazao ya kimkakati ya nafaka, jamiii ya mikunde na mafuta, pia, itatafiti na kupendekeza teknolojia mpya 10 za kanuni bora za kilimo katika nyanja za afya  ya udongo, magonjwa, wadudu  na viuatilifu vya kudhibiti visumbufu vya mimea. Vilevile, TARI itatafiti na kupendekeza teknolojia tano  za kuongeza thamani ya mazao ya maharage, miwa, soya, viazi lishe na korosho.
  • Ili kuimarisha upatikanaji wa mbegu na miche bora, TARI itazalisha mbegu za awali miche/vikonyo/pingili milioni 37.5 na kusambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku na kukamilisha ujenzi wa ghala tano zenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 2,075 katika vituo vitano vya TARI. Ujenzi huo utakapokamilika TARI itakuwa na uwezo wa kuhifadhi mbegu za awali tani 4,565 zenye uwezo wa kuzalisha mbegu za msingi tani 45,650 zenye uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 1,369,500 ya mbegu zilizothibitishwa
  • Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuongeza eneo la umwagiliaji lenye jumla ya hekta 256,185.46 kwa kukamilisha ujenzi wa skimu, kukarabati skimu zilizochakaa, kujenga skimu mpya na mabwawa 100 kwa ajili ya umwagiliaji.
  • Katika mwaka 2023/2024, Tume imepanga kukamilisha ujenzi wa miradi 25 na ukarabati wa skimu 30 zenye jumla ya hekta 95,005 pamoja na mabwawa 14 yenye mita za ujazo 131,535,000; na kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu 42 na mabonde ya kimkakati 22 ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2022/2023.
  • Tume imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa  mabwawa mapya 100 na kuanza ujenzi wa mabwawa hayo yenye takribani mita za ujazo 936,535,700; kuanza ujenzi na kukarabati skimu 59 zenye jumla ya hekta 143,482
  • Tume imepanga kuanza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde 22 ya umwagiliaji yenye ukubwa wa hekta 306,361. Baadhi ya mabonde hayo ni eneo la ziwa Victoria, Tanganyika, Rufiji, Manonga – Wembere, Bugwema, Lukuledi, Songwe na Ruvuma

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa