Wakulima wapimiwe ardhi na wapewe hati, asema Naibu wa Waziri Mavunde

Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe. Anthony Mavunde ameitaka Timu ya wataalamu wa Ardhi na Halmashauri ya Wilaya za Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya shughuli za Kilimo wakati wa ushughulikiaji na utatuzi wa migogoro ya Ardhi na kuyapima maeneo sambamba na utoaji wa hati za mashamba.

Naibu Waziri Mavunde amezungumza hayo leo tarehe kwenye mkutano wa hadhara uliohusisha Kamati ya Mawaziri Nane wa Kisekta inayoshughulikia migogoro ya Ardhi kwa Vijiji 975 uliofanyika kwenye Kitongoji cha Nkanka, Kijiji cha Itumba Wilayani Ileje Mkoani Songwe.

“Sisi tunao mkakati maalumu wa kuja na mfumo wa Kilimo cha pamoja ‘Block Farming’ ambapo hivi sasa tunayo mashamba makubwa 110 Nchi nzima na tunategemea ifikapo Mwaka 2030 tuwe na Mashamba makubwa yapatayo 10,000. Hivyo, niwaombe, wale wote ambao mtahusika kwenye utekelezaji wa maamuzi haya ya Baraza la Mawaziri, muhakikishe mnatekeleza mpango wa matumizi bora ya Ardhi na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za Kilimo. Msiishie kuyatenga tu lakini pia hakikisheni pia mnayapima na kuwapatia hati za umiliki wa mashamba yao. Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kumuona kila mkulima ananufaika na kilimo hivyo kupitia fursa hii ya kupata hati za mashamba itawawezesha pia kupata mikopo kupitia Taasisi mbalimbali za kifedha,” alisema Mavunde.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Mawaziri Nane wa Kisekta, Mhe. Dkt. Angeline Mabula amezitaka mamlaka za Mikoa, kutenga maeneo ya Ardhi kwa ajili ya Shughuli za Kilimo na Mifugo.

“Tunaamini kila Mkoa una maeneo ambayo yanafaa kwa Shughuli za Kilimo, Mifugo na Uwekezaji, hivyo basi tuyarasimishe kwa kuyapima pamoja na kuyapatia Hati za umiliki. Makamishna wa Ardhi wa Mikoa na Maafisa Ardhi, muache kufikiri tu katika upimaji wa viwanja pekee,” alisisitiza Mhe. Mabula.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa