Tanzania na Israel kushirikiana kwenye ujuzi wa uzalishaji wa mbegu

Waziri wa Kilimo wa Israel Oded Forer na Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe. Anthony Mavunde.

Nchi za Tanzania na Israel zimeanzisha mazungumzo kuelekea katika makubaliano ya kushirikiana katika maeneo ya uzalishaji wa mbegu na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Hayo yalizungumzwa Jijini Tel Aviv,Israel wakati wa mkutano baina ya Waziri wa Kilimo wa Israel Mhe. Oded Forer na Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe. Anthony Mavunde.

Akizungumza katika Mkutano huo, Waziri Forer ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kudhamiria kuboresha sekta ya kilimo nchini Tanzania kupitia kauli mbiu ya Ajenda 10/30 na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kuongeza ujuzi na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye maeneo ya uzalishaji mbegu na kilimo cha umwagiliaji ili kuiwezesha nchi ya Tanzania kufikia malengo yake.

“Tumekuwa na mahusiano mazuri na Tanzania kwa muda mrefu,ninaona wajibu wetu wa kusaidiana na serikali ya Tanzania katika kuboresha kilimo hasa katika maeneo ya uzalishaji wa mbegu bora na kilimo cha umwagiliaji hivyo mtegemee ushirikiano wa dhati kutoka Serikali ya Israel hasa katika kuwajengea uwezo wataalamu wenu kupitia mafunzo mbalimbali,” alisema Forer.

Akielezea vipaumbele vya Wizara ya Kilimo nchini Tanzania ,Naibu Waziri Mavunde aliainisha juu ya msukumo mkubwa uliopo katika uzalishaji wa mbegu bora, kuimarisha Utafiti wa Kilimo,Uwekezaji katika kilimo cha Umwagiliaji na Programu ya kushirikisha vijana katika kilimo(BBT) maeneo ambayo ameiomba serikali ya Israel kusaidia katika kuwajengea uwezo Watanzania kupitia mafunzo na matumizi ya teknolojia mbalimbali ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Kabla ya mkutano huo,Naibu Waziri Mavunde akiongozana na Balozi wa Tanzania Nchini Israel Mhe.Alex Gabriel Kallua alipata nafasi ya kutembelea Kampuni za utengenezaji wa greenhouse na shamba la mkulima wa zabibu.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa