Katibu Mkuuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ameitembelea Taasisi inayojishughulisha na mazao ya bustani na vikolezo TAHA ( Tanzania Horticulture Association) iliyopo jijini Arusha baada ya kuvutiwa na utendaji wake wa kazi.
Kusaya amesema kwamba hii yote ni kazi nzuri ya Mhe. Rais John Joseph Magufuli kwa juhudi anazozifanya kufungua fursa kwa Taasisi na Sekta binafsi ili kuziwezesha kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kuisaidia Serikali kodi ambazo zinafanya kazi mbalimbali kama vile ujenzi wa miundo mbinu ya barabara.
Aidha,Kusaya amewahakikishia TAHA kuwepo kwa ushirikiano mkubwa baina ya Wizara ya Kilimo na Taasisi hiyo katika mambo mazuri wanayofanya. Hata hivyo Taasisi inamsaidia mkulima kutoka katika hatua moja kwenda nyingine kwani kilimo ni ajira na uchumi na jitihada hizo zinaonesha kilimo ni ajira na inahamasisha vijana kujiunga kwenye kilimo.
“Vijana wana hamu ya kujikita kwenye kilimo hasa horticulture,mimi nitakuwa sehemu yenu zaidi msisite kunitafuta,Wizara tuna mpango wa kuandaa mkakati mpya wa horticulture kulingana na mazingira ya sasa na uliopo unaishia mwaka 2021.”alikaririwa akisema