Wizara ihakikishe kilimo kinasimamiwa kikamilifu-Waziri Hasunga

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amewaagiza watendaji Wakuu wa wizara na taasisi zake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Ametoa kauli hiyo leo alipofanya kikao kazi cha menejimenti iliyohusisha wakurugenzi wa wizara,bodi za mazao na wakala zilizo chini ya wizara hiyo jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa kazi za wizara.

Hasunga amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano wizara ya Kilimo imefanikiwa kuimarisha uzalishaji wa mazao hususan ya chakula hali iliyopelekea nchi kuwa na utoshelevu wa chakula kipindi chote.

“ Wizara ya Kilimo imefanya  mengi ya manufaa kwa kusimamia wakulima kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara hali iliyopelekea uchumi wa nchi kuimarika “ alisisitiza Waziri Hasunga

Katika kikao hicho cha mwisho katika mwaka mwa fedha 2020  Waziri Hasunga  alisema watendaji Wakuu wa wizara Taasisi watapimwa kwa  kuongeza uzalishaji  mazao ya kilimo ,pili idadi ya ajira zitakazozalishwa kwenye mnyororo wa thamani wa zao,

Tatu mchango wa zao katika upatikanaji wa fedha za kigeni, na nne idadi ya wakulima na kiasi cha ekari wanachozalisha.

Hasunga aliongeza kuwa Bodi za mazao zitapimwa kwa mashamba bora ya mfano waliyonayo,sita idadi ya viwanda vinavyochakata mazao ya Kilimo na mwisho idadi ya masoko  kwa mazao ya wakulima

Amezielekeza bodi za mazao na taasisi zote kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri wa kuepusha kero za wakulima kuhusu upatikanaji wa mbegu bora,pembejeo,viuatilifu na masoko ili wanufaike na kazi za Kilimo .

“Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza wizara ya Kilimo kuhakikisha inaondoa kero zote za wakulima kwa kuzitatua haraka katika ngazi zote hadi wilayani ili asiwepo mtu yeyote atakayekuwa kikwazo kwa wakulima nchini” amesisitiza Waziri Hasunga

Katika kikao kazi hicho Waziri huyo wa amesisitiza kuwa serikali haitopanga bei za mazao ya pamba,mahindi mpunga au ufuta bali itahakikisha wakulima wanapata bei nzuri ya soko.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema watumishi na watendaji wa wizara wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ubunifu ili wakulima nchini wanufaike .

Kusaya alisema ataendelea kusimamia na kufuatilia utendaji kazi wa watendaji wakuu na taasisi zake ili malengo ya Serikali na maagizo yote yapatiwe utekelezaji ili uzalishaji na tija kwa mazao ya wakulima nchini uongezeke.

Kikao kazi hicho kilihudhuriwa pia na Manaibu Waziri Hussein Bashe na Omary Mgumba ambao walitumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi kwa ushirikiano walioutoa kwa Mawaziri kwa kipindi chote walichofanya kazi wizarani hapo

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa