Vyuo vya kilimo nchini Tanzania vyatakiwa kujiimarisha kimapato

Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo ( MATI) vimeagizwa kuhakikisha vinatumia wataalam wakufunzi na rasilimali ardhi kuzalisha mazao mengi bora ili kuwa na uhakika wa kipato na kujiendesha kibiashara.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya wakati alipotembelea Chuo cha Kilimo Mubondo Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma.

” Tumieni sayansi kuzalisha mazao ya kilimo kwa kuhakikisha mnapima udongo na kujua virutubishi vinavyofaa ili mjue zao gani na aina gani ya mbolea ili kuwa na mavuno ya kutosha kuwezesha vyuo kujipatia mapato ” Kusaya

Katibu Mkuu huyo alisema lengo la serikali kuanzisha vyuo vya mafunzo ya kilimo ni kufundisha vijana na wakulima wengi kanuni bora za kilimo ili waweze kutoa mchango katika kukuza sekta ya kilimo nchini.

Amevitaka vyuo hivyo kutumia vema ardhi iliyopo na teknolojia  kutoa mafunzo bora na kuzalisha mazao kibiashara  ili wanafunzi wanaohitimu waweze kuwa mahili katika kujitegemea na kuongeza ajira kupitia kilimo na chuo kupata mapato .

” Vijana wengi watakapofanya vema na kufanikiwa katika kuanzisha shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo ndio itakuwa nafasi ya vyuo hivi kujitangaza na kuvutia vijana wengine na wakulima kuja kujifunza ” alisisitiza Katibu Mkuu huyo

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kilimo MATI Mubondo Hanif Nzury aliomba serikali ikipatie Chuo hicho trekta ili kiweze kutumia kuongeza uzalishaji zaidi wa mahindi, alizeti na michikichi ombi ambalo Katibu Mkuu alilikubali na kuahidi kulifanyia kazi.

Aidha Katibu Mkuu Kilimo amewataka Maafisa Ugani kote nchini kuwasaidia wakulima kwa kuwatembelea na kuwapa ushauri juu ya kanuni bora za kilimo .

Katika hatua nyingine Kusaya ameziagiza taasisi zote chini ya Wizara ya Kilimo kuhakikisha wanashirikiana na Halmashauri nchini kupima maeneo hayo na kupata hatimiliki ikiwa na lengo la  kuyaepusha na uvamizi toka kwa wananchi

Wizara ya Kilimo inasimamia vyuo 14 vinavyotoa Mafunzo ya stashahada (Diploma) na astashahada ( Certificate)  pamoja na vituo vya utafiti 17 nchini.

Awali Katibu Mkuu Kusaya alitembelea Shamba la mbegu bora la Bugaga lililopo Kasulu chini wa Walaka wa Mbegu (ASA) ambapo ameagiza wahakikishe miche 5000 ya michikichi iliyopo tayari hapa kituoni inawafikia wakulima kama alivyoagiza Waziri Mkuu.

“ Waziri Mkuu yuko mstari wa mbele kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mafuta ya kula hivyo endeleeni kuzalisha miche mingi ya michikichi ili wakulima wapande na hatimaye tupate mavuno mengi yatakayotosheleza mahitaji ya mafuta” alisema Kusaya.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa