Vyuo Tanzania vyahimizwa kutoa mfano katika kilimo

Serikali imewataka wahitimu wa vyuo vya kilimo kote nchini kutumia fursa ya uhaba wa maafisa ugani ulioko nchini kwa kwenda kutoa elimu kwa wakulima na kuanzisha mashamba ya mfano kwa wakulima

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana wakulima mkoani Arusha uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Rose Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omari Mgumba amesema kwamba maafisa ugani wafungue mashamba ya mfano na watoe huduma kwa wakulima kama sehemu ya kujiajiri .

“Sasa hivi kilimo kimebadilika wapo watu ambao wanazunguka kuwatafuta wataalamu wa kilimo ili wakapate huduma kwenye shughuli zao na wapo tayari kulipia wataalamu lakini wagani hawapatikani. Alisema Mhe Omari Mgumba.

Amewataka vijana kuwekeza kwenye Uzalishaji wa mbegu bora za mazao nchini kwani kuna uhitaji mkubwa wa mbegu nchini.

Akitolea mfano amebainisha kwamba mahitaji ya mbegu ni tani 187,000 kwa mwaka wakati uzalishaji wa ndani ni tani 71,000 hivyo amewataka vijana kutumia fursa hiyo kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu hasa za mazao ya bustani na maua katika ukanda huuwa kaskazini ambao unajumuisha mikoa ya Arusha,Tanga,Kilimanjaro na Manyara.

Hata hivyo amebainisha kwamba jumla ya vijana hapa nchini ni milioni 16.1 sawa na asilimia 35 ya idadi ya watu wote, Kwa mujibu wa Utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa wa mwaka 2014, nguvu kazi ya vijana ni asilimia 67.1 ya nguvu kazi yote ya Taifa na kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 11.7 ya nguvu kazi yote.

“ Takwimu hizi zinaonesha umuhimu wa Nguvu Kazi ya Vijana na Sekta ya Kilimo kwa maendeleo ya Taifa” Alibainisha Mhe Mgumba.

Aidha amesema kilimo ndio sekta pekee ambayo haibagui mtu aliyesoma na asiyesoma kwani kilimo kinahitaji elimu kidogo sana na unapata utajiri kupitia kilimo alisisitiza Mhe. Mgumba

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Mkakati wa Miaka Mitano wa Taifa kwa Vijana kushiriki katika sekta ya kilimo wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21. Utekelezaji wa Mkakati huo unahusu masuala ya ardhi ya kilimo, rasilimali fedha kwa ajili ya kilimo, pembejeo na zana za kilimo, masoko ya mazao ya kilimo, mabadiliko ya tabianchi, ujasiliamali .

Hata hivyo alibainisha kwamba Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana ambapo tayari inatekeleza Mkakati wa Kupunguza Upotevu wa Mazao Baada ya Kuvunwa na takwimu zinaonesha upotevu wa mazao yasiyo ya nafaka ni asilimia kati ya 30-40 ili kupunguza hasara kwa mkulima.

Aidha, Naibu Waziri amefafanua kwamba Wizara ya Kilimo kupitia TPRI itaendelea kutoa mafunzo ya matumizi bora ya viuatilifu kwa wakulima na wafanyabiashara nchi nzima ili kuhakikisha matumizi bora ya viuatilifu na afya ya mimea ili kumsaidia mkulima.

“TPRI imeendelea kusajili viuatilifu, kufanya ukaguzi wa pembejeo zisizofaa kwa matumizi ya kilimo kwa wafanyabiashara wasiowaaminifu na kutoa elimu kwa wakulima ili wasipate hasara za kutumia viuatilifu visivyo na ubora” Amesema Mhe. Mgumba

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa