Juhudi zinazochukuliwa na Serikali zimewezesha uzalishaji wa zao la mkonge kupanda kutoka tani 19,700 mwaka 1970 hadi tani 36,000 kufikia Desemba 2019. Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba
Ameongeza kuwa takwimu hizo zinajumuisha mkonge unaozalishwa na wakulima wakubwa (Estates) ambao huzalisha takriban tani 28,000 na wakulima wadogo ambao huzalisha takriban Tani 8,600. Aidha amesema hata hivyo, uzalishaji huu hauridhishi ikilinganishwa na fursa zilizopo kwenye Tasnia ya Mkonge kutokana na mahitaji makubwa ya zao hilo duniani.
Mgumba amesema Serikali imejipanga kuongeza tija na uzalishaji kwa kuanzisha vitalu vya mbegu ya mkonge katika Halmashauri zote amabako zao la mkonge linastawi. Aidha, amebainisha kwamba kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano uzalishaji wa mbegu bora umeanza ili ziweze kuzalishwa kwa wingi na kufanya uhakiki wa mashamba ya Mkonge yaliyobinafsishwa ili yaweze kuzalisha mkonge .