Lengo ni kupata twakimu kwa upangaji mwafaka
Serikali ya Tanzania imetangaza usajili wa wadau wote katika mnyororo mzima wa uongezaji thamani ya mazao ya kilimo.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema kuwa lengo la usajili huo ni kupata takwimu sahihi ya wadau mbalimbali wanaotoa huduma katika sekta ya kilimo nchini. Hawa ni wakulima, watoa huduma mbalimbali za pembejeo, wasindikaji, wafanya biashara za mazao, taasisi za fedha, watoa huduma wa sekta binafsi katika kilimo kama asasi za kiraia na mashirika ya ndani na nje ya nchi yanayotoa huduma kwenye kilimo, wenye viwanda vya kuongeza thamani, watengenezaji, wauzaji na wasambazaji wa zana za kilimo na kadhalika.
Usajili huo utafanyika kwa njia ya kidigitali kwenye mtandao wa www.kilimo.go.tz na kupitia simu za kiganjani. Unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 Februari, 2020 na kukamilika tarehe 14 Aprili, 2020. Kupitia usajili huo, takwimu na taarifa muhimu zitapatikana kwa ajili ya kuendeleza kilimo zikiwemo watoa huduma za pembejeo, huduma za ugani, taasisi za fedha, wasindikaji na wenye viwanda, watengenezaji, wauzaji, wasambazaji wa zana za kilimo, na hivyo, kuweza kujua kiwango cha uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Waziri Hasunga amesema kuwa Wizara ya Kilimo inaendelea na usajili wa wakulima kote nchini ili kuweza kuwatambua na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, mitaji kwa ajili ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo na kupata taarifa sahihi za uzalishaji. Awamu ya kwanza ya wakulima kufikia Januari, 2020 ilionyesha jumla ya wakulima 1,279,884 na usajili bado unaendelea.
Kati ya hao, wakulima wa mashamba makubwa ni 147. Wakulima wa zao la kahawa ni 101, wa chai ni 12, wa mkonge 22 na miwa 12.
Wakulima wadogo ni 1,279,737 wakiwemo 309,000 wa zao la korosho (98.4%), 305,260 wa kahawa (95.4), pareto 10,687 (112%), mkonge 6,885 (91%). Wakulima wa miwa walikuwa 6,745 (96.4), chai wakulima 31,092, tumbaku wakulima 53,757 (107.5%) na pamba wakulima 556,306 (92.7).
Wakati huo Waziri Hasunga amesema kuwa maendeleo ya kilimo hasa katika kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima yanategemea kwa kiasi kikubwa matumizi sahihi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu. Licha ya umuhimu huo, bado kuna changamoto ya upatikanaji na matumizi sahihi ya pembejeo hizo ikilinganishwa na mahitaji.
Aidha, inakadiriwa kuwa wakulima nchini Tanzania wanapoteza takribani asilimia 30 ya mazao kabla na baada ya mavuno kutokana na magonjwa na milipuko ya visumbufu mbalimbali vya mimea.