Tumieni ongezeko la uzalishaji wa mpunga kwenye mradi wa TANRICE kama chachu – Mhandisi Mtigumwe


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe amewaasa Wataalam wa Sekta ya Kilimo kuongeza uzalishaji na tija kwenye zao la mpunga kwa kutumia mafanikio yaliyojitokeza kwenye utekelezaji wa Mradi wa Kuongeza Uzalishaji na Tija kwenye zao Mpunga Awamu ya Pili (TANRICE 2).
Mhandisi Mathew Mtigumwe ameyasema hayo wakati wa mkutano wa kupitia namna Wizara ya Kilimo na Wadau mbalimbali walivyotekeleza Mradi wa TANRICE 2, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.
Mhandisi Mtigumwe amesema wakati wa utekelezaji wa Mradi wa TANRICE 2 chini ya ufadhiri wa Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) uzalishaji wa zao la mpunga kwenye mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro uzalishaji umeongezeka kutoka tani 3.2 kwa hekta mwaka 2012/2013 hadi tani 4.6 kwa hekta mwaka 2018/2019.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe


“Ninatambua, juhudi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la JICA kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga kwa Wakulima katika skimu za umwagiliaji hapa nchini, Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo hakikisheni kwamba mafanikio haya, yanatumika kama chachu na yaenezwe kwa Wakulima wengi, kote nchini”. Amekaririwa Eng. Mtigumwe.
Mradi wa TANRICE 2 umekuwa ukitekelezwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Morogoro na kwa kipindi cha miaka mitano ambapo jumla ya shilingi milioni 500 ziliwekezwa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo cha mpunga.
Mkutano huo pia uliudhuliwa na Mwakilishi wa Shirika la JICA Tanzania, Bwana Kentaro Akutsu, Mratibu Mkuu wa Mradi wa TANRICE 2, Bwana Kenji Shiraisha pamoja na Dkt. Zaki Mohamed Abubakar Mkuu wa Kitivo cha Shule ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar pamoja na Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vilivyo chini ya Wizara ya Kilimo.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa