Tanzania kuongeza uzalishaji wa mkonge

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji imeipongeza serikali ya Tanzania kwa mikakati yake madhubuti ya kuinua zao la mkonge nchini na kuridhishwa na hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na serikali katika kuongeza uzalishaji wa Mkonge kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji Dr.Christine Ishengoma wakati za ziara ya kamati kukagua ukarabati wa jengo la ofisi ya Bodi ya Mkonge na kutembelea wasindikaji na wakulima wa mkonge katika Wilaya za Muheza na Korogwe.

Mkonge House Tanzania

“Hili jengo limejengwa mwaka 1840,lakini ukarabati huu umelifanya liwe na taswira tofauti ya kuvutia.Ukarabati huu umetumia kiasi cha Tsh 506m katika hatua hizi mbili za awali gharama ambayo usingeitemea kutumika kutokana na hali ya uchakavu wa majengo haya.Tunaiona mikakati mizuri ya serikali katika kuchochea uzalishaji wa zao la mkonge,tunapongeza jitihada hizi na sisi kama kamati ya bunge tutatoa ushirikiano kuhakikisha tunafikia malengo ya kukuza tasnia hii ya mkonge.Serikali lazima ihakikishe inasimamia vyema zao hili kwa kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili wakulima wa zao hili wanufaike na kilimo chao,” alisema Dr. Ishengoma.

Akijibu changamoto za wakulima,Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde amebainisha mikakati ya serikali katika kukuza zao la mkonge ikiwemo ununuzi wa korona mpya za kisasa ili zisaidie kusindika mkonge mwingi kwa wakati muafaka tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo mkonge mwingi wa mkulima hukaukia shambani kwa kushindwa kuvunwa kwa wakati na hivyo kupelekea hasara kwa mkulima.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Ndg. Saddy Kambona amesema kwamba mpango wa sasa wa Bodi ni kuhakikisha wanaongeza uzalishaji kuwa mkubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya masoko mbalimbali ya nje ya nchi hali ambayo itasaidia kukuza pato la taifa na kuinua uchumi wa wakulima.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa