Serikali yatenga bilioni 16 kujenga kituo mahiri cha usimamizi wa mazao ya nafaka

Katibu Mkuu wa Kilimo Bw. Gerald Kusaya leo (19/06/2020) amesaini mkataba wa ujenzi wa kituo mahiri cha usimamizi wa mazao ya nafaka jijini Dodoma ambapo alisaini pamoja na  Kampuni ya M/S BJ Amuli Architect ambayo ilishinda zabuni ya kufanya ubunifu katika eneo la ujenzi. Ujenzi huo utagharimu  kiasi cha shilingi billion 16 hadi kukamilika kwa ujenzi wa kituo.

Aidha, Kusaya amesema mradi wa TANIPAC unatekelezwa katika mikoa 10 ndani ya halmashauri 18 Tanzania Bara na serikali inategemea kujenga maghala 14 katika kituo hicho kitakachojengwa Mtanana B katika halmashauri ya Kongwa jijini Dodoma.

“Tunalenga zaidi usalama wa chakula na ni mapenzi ya Rais ndio maana ametoa hizi pesa kupambana na sumukuvu” alisema Kusaya

Hata hivyo Kusaya amesema eneo hilo la hekari 150 kitajengwa Kituo mahiri cha usimamizi wa mazao ya nafaka na vihenge ambapo kituo hicho kitakuwa ni cha mafunzo ya kupambana na sumukuvu.

Katika maelezo yake Kusaya amemtaka mshauri elekezi wa kampuni hiyo Bw. Nathaniel N. Alute kumaliza kazi kwa wakati ili kuepuka kuongezeka kwa gharama kwani kazi yake kubwa ni kufanya ubunifu wa ujenzi wa kituo na anatumaini kuwa kazi itakuwa nzuri kwani kituo kikubwa.

“Nahitaji kuona unafanya hii kazi kwa umahiri na kufanya ubunifu,ufanye kwa wakati na kazi bora,ufanye ndani ya wakati ili isiongezeke gharama ya ujenzi “ alisema Kusaya

Aidha, Kusaya ameeleza kuwa wananchi wa mtanana wametoa  ardhi yao bila fidia na nia yao kubwa ni kuona mradi unaenda na wanahitaji kituo ili waweze kupata mafunzo ya namna ya kutunza mazao yao vizuri.

Mshauri elekezi wa kampuni ya BJ Amuli Architect  Bw.Nathaeli ameshukuru kwa kupata fursa hiyo na kuomba ushirikiano na Wizara ili kazi iende vizuri na kukamilika kwa wakati kwani muda waliopewa ni wa miezi mine kwa mujibu wa mkataba.

Hata hivyo amesema watajitahidi  kufanya kazi kama inavyohitajika pamoja na kufanya ubunifu wa majengo yanayohitajika kulingana na ramani ya kituo watakayopewa. Ubunifu huo wa majengo utaanza rasmi kuanzia tarehe 26/06/2020 hadi tarehe 26/10/2020 ndipo atakapotakiwa kukabidhi kazi hiyo.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa