Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Mhe. Anthony Mavunde amewataka Wakulima wa zao la mkonge kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo kwani serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaweka mazingira bora yatakayomsaidia mkulima wa mkonge kuzalisha kwa tija na kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa mkonge kufikia tani 120,000 kwa mwaka 2025/26.
Naibu Waziri Mavunde aliyasema haya katika mkutano wa tatu wa wadau wa Sekta ya Mkonge uliofanyika jijini Tanga akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB).
Alisema katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2022- 2023, serikali imeongeza bajeti ya utafiti na uzalishaji mbegu bora kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kuongeza uzalishaji wa miche ya mkonge kufikia miche 10,000,000, kuboresha maabara ya kituo cha Utafiti TARI Mlingano, kufanya utafiti juu ya mbegu bora zenye ukinzani wa magonjwa ikiwa ni pamoja na kusambaza matokeo ya tafiti kwa wakulima na kutoa huduma za ugani.
“Moja ya changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa mkonge ni upungufu wa makorona unaopelekea mkonge kuvunwa mara moja kwa mwaka badala ya mara mbili, na hivyo kusababisha hasara kubwa kutokana na mkonge kuozea shambani. Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022 – 2023 Serikali imepanga kununua Korona tatu (3) za kuchakata Mkonge Ili kuwawezesha wakulima kuongeza uwezo wa kuchakata mikonge yao pindi wakivuna na kuepusha kuozea Mashambani,” alisema Mavunde.
Pia, Mhe. Mavunde ameitaka Bodi ya Mkonge kushirikiana na wadau wote kwenye mnyororo wa thamani kuweza kubuni bidhaa mbalimbali zinazotokana na mkonge kama vifaa vya ujenzi, bidhaa mbadala wa mbao, sukari ya mkonge, pombe ya mkonge, karatasi maalum, bio gas, mbolea na chakula cha mifugo. Hatua hiyo, itapelekea kuongeza thamani ya zao la mkonge kwa kumnufaisha mkulima kupitia bei nzuri na pato la taifa kwa ujumla.