Kusaya: agizo la waziri mkuu kuhusu mbegu bora za michikichi Tanzania latekelezwa kigoma

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo amewapongeza watafiti wa mbegu za michikichi kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora na kuwataka  watumie muda mfupi zaidi wa kuzalisha na kuzisambaza kwa wakulima nchini

Agizo hilo lilitolewa mjini Kigoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerald Kusaya wakati alipotembelea kukagua kituo cha Utafiti wa kilimo ( TARI) Kihinga, Gereza Kwitanga na JKT Bulombola zenye jukumu la kuzalisha miche bora ya michikichi aina ya Tenera.

KM CHIKICHI

“ Watafiti endeleeni na utafiti wa kupunguza muda wa kuzalisha mbegu bora toka miezi 18 hadi chini ya mwaka mmoja ili wakulime wapate mbegu hizo kwa wingi waongeze uzalishaji kufikia lengo lililowekwa la miche milioni tano kwa mwaka” alisema Kusaya

Kusaya alisema ametembelea mkoa wa Kigoma kufanya ufuatiliaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilitoa mwezi Agosti mwaka 2018 la kuitaka wizara ya kilimo kuzalisha miche bora ya michikichi milioni 20 kwa kipindi cha miaka minne na kugawa kwenye halmashauri za mkoa huo na mikoa mingine ili nchi ipate mafuta ya kutosha ya kula.

Katibu Mkuu huyo alisema ni lengo la serikali kuona zao la michikichi linalimwa mikoa mingi zaidi na ili kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini kwani zao hilo ndio tegemeo kubwa la viwanda vya mafuta..

Awali Kusaya alisema kwa sasa Tanzania inatumia shilingi Bilioni 443 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi kutokana na uzalishaji wa mazao ya mafuta kuwa mdogo .

“ Kwa mwaka nchi inahitaji mafuta ya kula tani 570,000 wakati uzalishaji wa ndani ni tani 250,000 sawa asilimia 36  hivyo kuwa na upungufu wa tani 220,000  “ alisema Katibu Mkuu huyo

Awali akiwasilisha taarifa ya Kituo cha TARI Kihinga Mkurugenzi Mkuu wa TARI Geofrey Mkamilo alisema agizo la Waziri Mkuu limeanza kutekelezwa kwani kufikia Mwezi Aprili mwaka 2020 jumla ya mbegu bora za michikichi 1,791,768 ambazo zinaweza kupandwa kwenye eneo la ekari 35,835.

Dkt.Mkamilo aliongeza kusema jumla ya mbegu  za michikichi aina ya Tenera 1,255,111 na miche bora 167,315 imezalishwa na taasisi za umma na binafsi kutekeleza agizo la Waziri Mkuu.Mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno tani 5 kwa hekta .

Nae Mkuu wa Gereza Kihinga SSP Dominic Kazmil alimweleza Katibu Mkuu kuwa jumla ya mbegu 273,050 zimezalishwa tayari na miche 8,050 ipo tayari kwenda kupandwa na wakulima kwenye halmashauri za Mkoa wa Kigoma .

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru Wizara ya Kilimo kwa jitihada za kuhakikisha mkoa wa Kigoma unakuwa kitovu cha uzalishaji miche ya zao la michikichi.

Katika ziara hii ya mkoa wa Kigoma Katibu Mkuu Kusaya ameuomba uongozi wa mkoa kuhamasisha wakulima pamoja na kuzalisha michikichi sasa waanze pia kuzalisha mazao kama mkonge na korosho ili kuongeza wigo wa mapato kwenye mazao ya biashara.

Kusaya alisema ni wakati sasa wataalam wa kilimo wakawaelimisha wakulima waongeze mazao mengine ya biashara kama korosho na mkonge ili kuwa na uhakika wa kipato kwani ardhi ya Kigoma inafaa na kuwa wizara yake ipo tayari kuleta mbegu bora za mkonge na korosho.

Share your views about this story

Related stories

Subscribe to Kilimo News

Get the latest agriculture news in East Africa