Serikali ya Tanzania imesema wakulima waliokusanya kahawa yao kwenye vyama vya ushirika mkoani Kagera wataanza kulipwa madeni yao mapema wiki hii.
Kauli hiyo ilitolewa Jijini Mwanza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya wakati alipoongoza kikao cha viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, mikoa ya Mwanza na Kagera na vyama vikuu vya Ushirika KDCU na KCU kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Kusaya alisema tangu msimu wa ununuzi wa kahawa ulipofunguliwa mwezi Juni mwaka huu jumla ya shilingi Biioni 32 tayari zimelipwa kwa wakulima wa mkoa wa Kagera kutokana na kukusanya tani 62,336 za kahawa ghafi na tani 31,168 za kahawa safi kwenye vyama vikuu vya ushirika na vile vya msingi.
“Pamoja na kulipa Bilioni 32 za wakulima bado Chama Kikuu cha Ushirika KDCU kinadaiwa shilingi Bilioni 12 kutokana na kukusanya kahawa ya wakulima ,hivyo kikao chetu leo tumekubaliana KDCU waanze kulipa wakulima shilingi Bilioni 7 zilizopo tayari kuanzia kesho na zingine Bilioni 5 zitalipwa mapema wiki ijayo” alisema Kusaya
Katibu Mkuu huyo alisema deni hilo linatokana na KDCU kuendelea kukusanya kahawa ya wakulima kufuatia uwepo wa mavuno mazuri ambapo takwimu zinaonesha wanakusanya kwa siku kahawa yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.7 kutoka kwa wakulima na tayari wamenunua kilo milioni 37.3 kati ya lengo la kilo milioni 45 za kahawa msimu huu.
Kuhusu Chama Kikuu cha Kagera ( KCU) ,Katibu Mkuu Kusaya alisema wanadaiwa na wakulima shilingi Bilioni 7.1 na kuwa wamekubaliana kuanza kulipa shilingi Bilioni 2 mapema wiki huku wakiendelea na kukusanya fedha toka kwa wanunuzi waliowauzia kahawa.
“Shilingi Bilioni 2 za wakulima waliouza kahawa KCU tumekubaliana zitaanza kulipwa wiki hii Kagera na kuwa zingine Bilioni 3 zitatolewa na mnunuzi aliyeuziwa kahawa na KCU katika muda mfupi ujao” alisisitiza Kusaya.
Kusaya aliongeza kusema serikali imejipanga kikamilifu kuona wakulima wa kahawa kote nchini wanalipwa fedha zao kwani mfumo unaotumika wa vyama vikuu na AMCOS kununulia kahawa ni wa uhakika na kuwa wakulima wawe na subira kipindi kifupi fedha zitapatikana kwani wanunuzi toka nje ya nchi wameanza kuonyesha nia ya kuja Tanzania kutokana na tatizo la korona kudhibitiwa .
“Kuchelewa kwa malipo ya wakulima wa kahawa hususan mkoa wa Kagera yametokana na vyama vikuu vya ushirika kuchelewa kuuza kahawa” alisema Kusaya na kuwa serikali ipo tayari kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa mikopo kwa vyama vya ushirika kununua kahawa na kulipa wakulima.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wanaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima kama alivyoelekeza Rais Dkt.John Pombe Magufuli.
Prof. Shemdoe alisema kwa sasa wanunuzi na wafanyabiashara binafsi wanaruhusiwa kununua kahawa toka vyama vikuu vya ushirika au vyama vya msingi (AMCOS) lakini wahakikishe wanatoa bei nzuri na yenye ushindani wa soko.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora alisema wakulima wa kahawa msimu huu wamepata bei nzuri karibu asilimia 75 ya bei ya soko la dunia na kuwa vyama vikuu vya Ushirika (KDCU) na (KCU) kwa mkoa wa Kagera wamefanya kazi nzuri kuwezesha wakulima kulipwa bei nzuri.
Prof.Kamuzora ametoa wito kwa watanzania kuwa na tabia ya kunywa kahawa ili kusaidia upatikanaji wa soko la kahawa ndani ya nchi tofauti na ilivyo sasa kahawa asilimia 93 inayozalishwa nchini inauzwa nje ya nchi.
Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege alisema wanunuzi binafsi wa kahawa wanaruhusiwa kununua lakini sharti waingie mikataba na vyama vya vikuu vya ushirika au AMCOS ili kuwa na uhakika wa bei nzuri kumfikia mkulima.
Dkt. Ndiege alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya ushirika nchini hususan mkoa wa Kagera kutoa kipaumbele cha malipo ya wakulima waliouza mapema kahawa yao kutokana na fedha zilizopatikana sasa na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha Makatibu Wakuu Kilimo na Viwanda .
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Kahawa Tanzania imeonesha makusanyo ya kahawa msimu wa 2020/2021 yamefikia jumla ya tani 79,245 (73%) za kahawa ghafi kati ya lengo la tani 108,000 na tani 44,695 (63 %) za kahawa safi kati ya lengo la tani 70,000.
Kahawa hiyo imekusanywa toka kwenye mikoa yote 17 inayolima zao la kahawa nchini.
Aidha bei ya kahawa kwa mkulima msimu huu imekuwa ikilipwa kwa utaratibu wa malipo ya awali kupitia vyama vyao vya ushirika ambapo mkulima analipwa kwa kilo shilingi 1,200 kahawa ya Robusta maganda (dry cherry) na shilingi 1,250 na 1,500 kahawa za Arabika maganda (parchment)