Serikali imewataka wazalishaji mbegu za mazao nchini Tanzania kuongeza uzalishaji na ubora ili nchi iepukane na utegemezi toka nje. Akizungumza katika kikao cha wadau wa mbegu mnamo Jumanne jijini Dodoma,Naibu Waziri wa Kilimo Husein Bashe alisema ili Tanzania ifikie malengo ya kukuza uzalishaji wenye tija katika kilimo lazima ijitegemee kwa mbegu. Amebainisha kuwa usalama wa chakula unategemea sana uwezo wa nchi kuzalisha mbegu za mazao ndani na si kutegemea wahisani. “Kuwa na nchi inayotegemea mbegu za mazao toka nje kunaondoa dhana ya uhuru na kujitegemea,hivyo kuhatarisha usalama wa chakula na taifa” alisisitiza Naibu Waziri Bashe. Bashe aliwaeleza wadau hao kuwa Wizara ya Kilimo ina lengo la kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mbegu hususan zinazozalishwa nchini. Aliziagiza Taasisi za Utafiti wa
Kilimo(TARI), Kampuni ya Mbegu (ASA) kushirikiana na wadau binafsi kuwekeza mitaji ili kuinua uzalishaji wa mbegu bora ili kukidhi mahitaji ya wakulima. “Ni budi sasa taasisi zetu za TARI na ASA zikaanza kuzalisha mbegu mara tatu kwa mwaka kwenye mashamba kwa njia ya umwagiliaji badala ya kutegemea mvua “ Naibu Waziri alisema. Bashe alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina utegemezi wa mbegu asilimia 60 kutoka nje ya nchi. Hali hiyo imesababisha mbegu nyingi kuuzwa kwa bei kubwa na zingine kulalamikiwa na wakulima kuwa na ubora mdogo. Naibu Waziri Bashe aliwataka wadau kutengeneza mpango maalum wa kuongeza uzalishaji kwani serikali pekee haiwezi kutokana na soko la mbegu kuwa kubwa. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao ,Wizara ya Kilimo Nyasebwa Chimagu alisema kikao hicho kitajadili kwa mapana changamoto za upatikanaji mbegu bora na mfumo mzuri wa usambazaji mbegu nchini. Nyasebwa aliongeza kusema kwa sasa wakulima wana malalamiko mengi kuhusu upungufu wa mbegu ,hivyo wizara na wadau wana jukumu la kutafuta majawabu mapema